Advertisement
HADITHI:LUKUNGU(UPANDE WA PILI WA SARAFU)MTUNZI: RAJONCE JOHN
MWANDISHI: RAJONCE JOHN
WHAT'SAPP:0673049321
UMRI:MIAKA 18
SEHEMU YA KWANZA.
Usiku mmoja wenye upepo zaidi ya siku nyingine za wiki hiyo, ulipelekea wakazi wa jiji la Dalaba kurejea majumbani kwao mapema, ungepita mitaani siku hiyo ilikuwa tofauti sana na siku nyingine kwani kawaida ya jiji hilo huwa na watu wa kuranda huku na kule wenye kufanya kazi masaa ishirini na manne. Shughuli nyingi za jiji hilo zilisimama kufuatisha maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu, kitengo cha kushughulika na majanga ya dharura hasa yale ya asili. Taarifa zilizotolewa na mamlaka ya hali ya hewa ya nchi ya Tikali ni kuwa siku hiyo kutakuwepo na kimbunga Kelvin kitakachovuma kutokea upande wa bahari ya Hindi kuelekea nchi kavu. Kuanzia majira ya saa kumi na moja jioni upepo ulizidi kuwa katika mwendo wa tofauti, vumbi jingi, lilifunika jiji la Dalaba watu wengi walishauriwa kufunga milango na madirisha kuzuia kuezuliwa kwa mapaa ya nyumba zao.
Jiji la Dalaba linapatikana ndani ya nchi ya Tikali iliyopo upande wa mashariki mwa nchi ya Tanzania. Mhasisi wa nchi hiyo changa ni aliekuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi ya Tanzania,John Senyagwa, kuzaliwa kwa nchi ya Tikali kulipunguza fukuto la mapigano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi ya Tanzania. Miaka thelathini na tano iliyopita nchi ya Tanzania ilipitishwa kwenye moto mkali wa mapigano ambayo yalianza kama kipele baada ya kukikuna kilizalisha kidonda kidogo na mwishoni likawa donda ndugu ambalo tiba yake aliileta John Senyagwa.
Kwa wakati huo nchi ya Tanzania ilikuwa chini ya raisi Wakute Wakute raisi ambae aliingia madarakani baada ya kuondolewa kwa raisi Hashimu Maganga(Tuliona kwenye kitabu cha ANGUKO KUBWA). Raisi Wakute Wakute na serikali yake waliwekeza nguvu nyingi za maendeleo upande wa magharibi mwa Tanzania kwani raisi huyo alikuwa anatokea mkoa wa Tabora. Tabora ilikuwa kitovu cha miradi mingi iliyostahili na isiyostahili yote ilipelekwa Tabora, huduma zote za kijamii zilipatikana kwa wingi Tabora,kipato cha mtu mmoja mmoja kiliongezeka sana huko Tabora, watu walipewa mitaji ya kuendesha maisha yao na kuufunika umaskini uliokuwa kwa miaka mingi ya zamani kabla ya utawala wa raisi Wakute Wakute. Upande mwingine ambao ulipewa nguvu zaidi ni mikoa ya kaskazini huko palikugunduliwa visima vya mafuta ambavyo vilipata uwekezaji mkubwa sana kutoka makampuni ya nje. Upande wa mikoa mitatu ya mashariki Dar es salaam, Pwani na Morogoro iliachwa solemba, miundombinu ilikuwa mibovu sana, maji na umeme vilikuwa vya mgao. Licha ya wananchi kupiga kelele na kulalamika serikali iliwageuzia mgongo hakuna ambae alijali tena kuhusu mikoa hiyo, wananchi walichoka kupigia kelele mitandaoni, uoga waliuficha kwapani waliingia mitaani kuandamana, kudai haki ya kutekelezewa mahitaji yao.
Serikali iliwajibu kwa ukali askari wenye silaha waliwafuata huko huko kwenye barabara walizokuwa wanachoma vitu mbalimbali. Askari walitumia nguvu zaidi, wananchi waliachiwa majeraha makubwa na vilema vya kudumu. Vilio vyao vilimfikia John Senyagwa aliekuwa uhamishoni nchini Kenya. John Senyagwa alijitahidi kumtafuta raisi Wakute Wakute ili wazungumze lakini mtu huyo alimfungia vioo. John Senyagwa alirejea nchini Tanzania kwa Siri sana akikwepa kukamatwa na vikosi vya raisi Wakute Wakute. Hali haikupoa maandamano yalizaa vita kati ya jeshi la serikali ya Wakute Wakute na watu wa John Senyagwa. Mapigano yalichukua muda mrefu miezi kumi na tatu mbeleni umoja wa mataifa kupitia ujumbe wake kwenye jumuiya ya umoja wa afrika na mashariki waliwaita mezani wababe hao wawili.
Majadiliano yalifanyika nchini Uganda kwa lengo la kuleta amani nchini Tanzania, vikao vizito viliendeshwa kwa siku mbili mfululizo na maazimio yaliyoamuliwa ni kuigawa nchi ya Tanzania. Mikoa mitatu ya upande wa mashariki yaani Morogoro, Dar es salaam, na Pwani iliunda nchi mpya, nchi ya Tikali na kukabidhiwa kwa John Senyagwa. Mikoa mingine ilisalia chini ya raisi Wakute Wakute ambae alikubaliana na jambo hilo kutokana na kubananishwa kwenye kona ya kutaka kufunguliwa mashitaka kwa uarifu wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu, salama yake ilikuwa kukubali mikoa hiyo kuondoka Tanzania kwa upande mwingine mikoa hiyo mitatu haikua na faida yeyote kwake, alishaua bandari ya Dar es salaam, meli kubwa za mizigo zilitua Tanga na Mtwara, jiji la Tanga liligeuka kitovu cha biashara kwa nchi ya Tanzania. Mafuta yaliyochimbwa Mwanza yalisafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Tanga. John Senyagwa akiwa na miaka sitini na tisa alianza kuijenga nchi, kwanza alibadili majina ya mikoa na yote kuyapa hadhi ya majiji. Dar es salaam iliitwa Dalaba, Pwani iliitwa Labe na Morogoro iliitwa Gutemala. Raisi John Senyagwa aliongoza kwa miaka mitano pekee na kuwaachia viongozi wengine miaka thelathini na tano mbeleni inatufikisha katika mwanzo wa Simulizi yetu hii bingwa.
MELLOW APARTMENT
Ni makazi yaliyojengwa na serikali ya nchi ya Tikali, kwa lengo la kuwasaidia watu wa kipato cha chini kuishi kwenye majengo hayo kwa kulipia gharama nafuu. Makazi hayo yalikuwa kwenye mpango wa shirika la nyumba la Tikali, mpango wa kulipanga upya jiji la Dalaba pia kuinua uchumi wa watu ambao uliharibiwa wakati wa vita dhidi ya nchi ya Tanzania. Kwenye makazi hayo chumba namba mia nane tisini(890) alionekana mwanaume mmoja akishtuka usingizini. Simu yake ilikuwa inatetemeka sana baada ya kuingia ujumbe, alipeleka mkono mezani na kuichukua simu kwa mkono mmoja, mkono mwingine alitumia kufikicha macho yake kuondoa tongotongo ili apate nafasi ya kuona vizuri.
"KINDEGE KIMENASA" ujumbe ulisomeka namna hiyo, mtumaji akiwa amehifadhiwa Kwa jina T072.
"Ooooouuuuuuuuuuuuuh hii nchi haiishiwi mambo" aliongea huku akijinyoosha viungo vya mwili mpaka pale vilivyokaa sawa alishuka chini. Macho yalikuwa ukutani kutazama saa, mshale mfupi ulikuwa kwenye nne na ule mrefu kwenye tatu( saa kumi na robo usiku).
Jonathan Sakewa alipenda kuitazama saa ya ukutani, kuliko saa ya kwenye simu, akiwepo nyumbani alifanya hivyo kuipa nguvu akili yake uwezo wa kuanza uchakatuaji mapema. Alieleleka chooni aliporejea alikuwa na mambo matatu ya kuyafanya, hiyo ilikuwa kawaida yake pale siku mpya inapoingia kwanza alifanya sala kwa Mungu anaemtambua kisha alifanya mazoezi ya kujiweka imara, mwili ulipopata joto na kujiona yuko sawa alikimbilia bafuni alioga, alipotoka alikaa mezani kupitia kurasa ishirini za kitabu cha KIU kilichoandikwa na mwandishi Rajonce John, alipenda kusoma sana maandishi ya mwandishi huyo kuchangamsha akili kwa visa mafumbo vilivyochorwa katika vitabu vyake mbalimbali vyenye umaarufu sana barani afrika na duniani kote.
"Mifuko ya watu ina fedha nyingi, huwezi kuhesabia fedha zilizopo kwenye mifuko ya watu wengine lakini unaweza kuzifanya ziwe zakwako. Hakikisha kila unachokifanya kifanye kwa umaridadi zaidi ya kawaida ya watu wengine, amini fedha zitakujia, mabenki makubwa yanawalipa wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kompyuta ili walinde taarifa zao za kibenki,
Wasanii wakubwa huwalipa fedha nyingi wazalishaji wa midundo(producer) endapo wanauwezo wa kuzalisha midundo mikali zaidi ya wazalishaji wengine na nyimbo ikaenda mbali zaidi. Watu hawakupi pesa Kwa huruma wanakupa pesa endapo utajua mambo, yaani utatumia akili na uwezo wako wote kuleta kitu kipya hapo utahamisha fedha kuja kwenye mifuko yako" Jonathan Sakewa alisoma maneno hayo ya mwisho na kukifunika kitabu chake, tayari alishaongeza kitu juu ya maisha ya utafutaji kuwa anapaswa kutumia uwezo wake wote ili kuhamisha fedha kutoka kwenye mifuko ya watu kwenda mfukoni mwake. Saa kumi na moja na dakika tano alikuwa ndani ya mavazi makuu kuu, suruali kubwa lenye matobotobo na shati kubwa lililouzidi mwili wake mara mbili, usoni alikuwa na sura tofauti na ile aliyoamka nayo kitandani, alikikamata kiroba kwa mkono wa kulia na kukilaza mgongoni alifunga mlango na kushuka chini kwa kutumia ngazi za jengo hilo, alitembea kwa hatua ndefu ndefu alipofika mahali fulani alitoa fimbo kwenye kiroba chake fimbo ilikuwa ndogo aliivuta na kuongezea urefu, mwendo ulibadilika, alitembea taratibu akipapasa njiani kwa kutumia fimbo kuepuka mashimo na vitu vya hatari njiani, alikuwa ndani ya upofu wa kuigiza lakini ilikuwa ngumu sana kwa mtu kumbaini. Kweli mjini akili mafanikio huja yenyewe, alitembea mpaka nje ya jengo kubwa la kuuza pikipiki liliitwa Kamota Motorcycle, jengo hilo lilikuwa likitazamana na tawi la benki ya TMB(Tikali Microfinance Bank) alitandika kiroba chake karibu na ombaomba wengine waliokuwa na ulemavu maeneo mbalimbali, alikaa juu ya kiroba kwa kukunja miguu yake vizuri mikono ilikuwa hewani kuombaomba Kwa watu waliokuwa wanapita mahali hapo.
"Nisaidieni, nisaidieni chochote ndugu zangu, Mwenyezi Mungu atawalipa, Mwenyezi Mungu atawaongeza" Jonathan Sakewa alipaza sauti yake maradufu akiamini itawafikia wapitaji. Jiji la Dalaba lilishaingia kwenye harakati zake za kila siku, watu walikuwa katika mbio za kuenda sambamba na muda ili jioni itakapoingia wawe na sababu ya kuingiza mkono kinywani, wapitaji waliosikia sauti ya Jonathan Sakewa waliangusha chochote kama sadaka ya kupalilia upambanaji wao wa siku. Ilikuwa asubuhi,mchana na jioni ilifikia jua lilielekea magharibi ya mbali, juu ya kiroba cha Jonathan Sakewa kulikuwa na sarafu nyingi sana. Ombaomba mwenye mguu mmoja alizitazama fedha hizo kwa macho ya uchu, alizitazama zake aliona amezidiwa parefu sana, alinyanyua magongo yake mawili alijikongoja mpaka alipokuwa amekaa Jonathan Sakewa. Aliyaweka magongo pembeni na kuchuchumaa mbele ya kiroba cha Jonathan Sakewa, alianza kuokota sarafu moja baada ya nyingine. Jonathan Sakewa aliekuwa anamwona ombaomba huyo, alimkamata shingo kwa nguvu na kuanza kumkaba, omba omba alijitahidi kuondoa mikono imara ya Jonathan Sakewa lakini hakuweza, Jonathan Sakewa alipoona anaweza kuua alimsukumiza kwa nguvu.
Ombaomba alianguka mzima mzima huku akikohoa baada ya kukabwa vilivyo, watu waliokuwa wanatazama malumbano hayo ya ombaomba waliishia kuangua vicheko, baada ya kushindwa jaribio lake ombaomba mwenye tamaa aliokota magongo na kurudi mahali pake. Jonathan Sakewa hakuwa na cha kupoteza alikusanya kila kilichokuwa cha kwake, fimbo ilimwongoza kuondoka eneo hilo, alitokea mtaa wa pili alitembea mpaka kwenye duka moja la nguo, muuzaji alipomwona alimpokea huku akitazama huku na kule, kisha waliingia ndani hakukua na mtu mwingine zaidi yao walielekea kwenye chumba cha kubadili nguo.
"Kuna jambo gani huku kiongozi wangu" Muuza duka aliongea akiwa ameinamisha kichwa kutoa heshima mbele ya Jonathan Sakewa.
"Kindege kimenasa Madiwe ndio maana nimekuja huku, naomba nguo za kubadili"
"Sawa kiongozi lakini usalama mlizingatia maana usalama wa taifa wanafanya kazi zaidi ya uwezo wao wa kawaida" Madiwe aliongea huku akimkabidhi kiongozi wake nguo za kubadili.
"Unahofu na uwezo wangu Madiwe?"
"Hapana kiongozi nisamehe"
"Ondoa hofu kila kitu kipo kwenye mhimili wake" Jonathan Sakewa alivaa suti ya rangi ya bluu, suti ilimkaa vyema mwilini, alichukua mafuta fulani na kuyapaka baada ya dakika tatu sura bandia ilitutumka, aliimenya na kuiondoa alikuwa kwenye sura yake halisi.
"Ninaelekea studio, huko nitatoa taarifa ambayo inaweza kutikisa jiji au nchi nzima, jiandae kwa lolote ambalo litatokea maana taarifa inaweza kuwagusa wengi ambao wanaweza kurusha mawe kutokea gizani au kwenye mwanga"
"Sawa Mkuu nimepokea" Madiwe alijibu huku akiinamisha kichwa kutoa heshima. Jonathan Sakewa aliaga na kutoka nje, kidani alichochukua kwenye shingo ya ombaomba ambae alikuja kumwibia kilikuwa mkononi mwake BMW nyeusi ilikuwa nje ikimngojea aliingia ndani yake. Mwendo wa dakika sabini kutokana na foleni ya jiji la Dalaba hasa usiku kutokana na watu kurudi nyumbani muda huo, aliweza kufika studio za redio maarufu WAKITAA FM. Jonathan Sakewa alikuwa ni mwajiriwa na mtangazaji bingwa kabisa wa redio hiyo, alipoingia ndani ya jengo hilo alikutana na meneja wa vipindi na matangazo wa redio hiyo, walipeana mikono kusalimiana baada ya salamu Jonathan Sakewa alikuwa na maneno ya kuzungumza.
"Meneja samahani naomba uzungumze na wafanyakazi wote, waaambie warejee nyumbani na asibaki mtu hata mmoja, hata hao walinzi wa nje wakapumzike na familia zao, Kuna kipindi nahitaji niendeshe nikiwa peke yangu ili asitokee yeyote akapoteza maisha kwasababu yangu, sitaki damu ya yeyote ilie juu yangu" Jonathan Sakewa aliongea maneno makavu, yakilenga dhumuni lake la kuwa mahali hapo.
"Jonathan umeanza tena, ni juzi tu tumefunguliwa kutoka kwenye kifungo cha miezi sita, leo unataka kuturudisha kule kule, hapana aiseeh tafuta mahali pengine pa kutolea taarifa yako" Meneja aliweka ugumu.
"Meneja hii taarifa niliyokuja nayo ni muhimu kuliko hata kazi yako, kama redio itafungiwa na wewe utaendelea kupokea mshahara shida iko wapi?"
"Mimi ni kiongozi wako, naomba nikupe kauli mbili, kauli ya kwanza maneno ya boss ni msahafu hayapingwi wala kuulizwa ulizwa na kauli ya pili rejea kwenye kauli ya kwanza"Meneja alisisitiza kuwa yeye ndio boss na maneno yake yalipaswa kufuatishwa.
"Mmmmh meneja nimekupa heshima kwa kukutaarifu ninachotaka kukifanya lakini naona unajiinua zaidi ya kimo chako na kusahau kuwa sisi wote ni waajiriwa, zungumza na mkurugenzi yeye ndie ataamua kipindi kiruke au kisiruke" Jonathan Sakewa aliongea bila hofu yeyote.
Meneja akiwa amefura kwa hasira alivuta simu na kuipiga kwa mkurugenzi wa redio, baada ya simu kupokelewa aliiweka sauti kubwa Ili maneno ya Mkurugenzi yasikike vizuri na wote wawili, baada ya salamu Meneja alianza kutema kilichomfanya apige simu.
"Bwana Jonathan Sakewa anataka kuturudisha kwenye vita ambayo hatujui faida ya kupigania, anataka kutupeleka kwenye kifungo cha redio kwa mara nyingine, muda huu anataka niwarudishe wafanyakazi nyumbani kisha yeye afanye ujinga wake wa kuvigusa visivyogusika, mimi nimeongea nae sana lakini moto wake hauzimiki naomba wewe kiongozi wetu zungumza nae labda atakusikiliza mkuu" Meneja aliongea kwa kushadadia.
"Mruhusu afanye kipindi chake, kama ametaka ninyi msihusike kwenye mabalaa yake, rudini nyumbani mwacheni yamkute mwenyewe"
"Lakini boss hii ni hatari sana"
"Nimesema mruhusu aondoke kwanza kesho ni siku ya kuwalipa mishahara yenu, nenda kapumzike na familia yako kungojea mshahara wa kesho" Mkurugenzi wa redio aliongea na kukata simu. Meneja aliondoka kwa hasira, maneno ya Mkurugenzi yalionesha kumpendelea Jonathan Sakewa na kumzalilisha yeye aliekuwa anatetea uhai wa redio yao. Jonathan Sakewa aliingia studio na meneja aliwapa taarifa wafanyakazi kuwa warudi nyumbani wakapumzike, redio ilibaki na mtu mmoja Jonathan Sakewa alikuwa mbele ya kipaza sauti saa tatu kamili alikuwa anawaarika wasikikizaje wake kutokea kona mbalimbali za nchi ya Tikali. Jonathan Sakewa akifahamika kwa jina la utangazaji Msago wa Mapulo aliendesha kipindi maarufu kinachofahamika kama Mapulo(Marungu), kipindi kiliegemea kwenye ufichuzi wa mambo ambayo watu wengi hawakuyafahamu, mambo ambayo yalifunikwa kwenye kiroba cheusi ambacho ilikuwa kazi kwa watu kuyafahamu kirahisi. Wasikikizaji walitega sikio Kwa umakini wakitaka kujua Msago wa Mapulo amekuja na jambo gani jipya ambalo lingefungua masikio yao.
"Moyo moyo moyo ni kiungo kidogo sana kwenye mwili wa mwanadamu ukubwa wake hauzidi hata ngumi ya mkono wake lakini ajabu unaweza kuyabeba na kutunza mengi ambayo hata mkono hauwezi kuyabeba, waliosema moyo ni pori nene hawakukosea, moyo wangu umebeba mengi sana ambayo leo nitawapunguzia machache, nitayasema kwasababu sitaki kufa na kihoro cha hili jambo kubwa niteme nisiteme" Jonathan Sakewa aliongea namna hiyo akiamini wasikikizaji wake upande wa pili watasema ateme maneno ambayo alikuja nayo usiku huo, Msago wa Mapulo alikuwa mbele ya wakati Kwa mambo mengi sana hivyo wasikikizaji walishindwa kumeza hata mate kwa shauku iliyowajaa mithiri ya kutaka kufulumia.
"Usiku huu, usiku huu ndani ya dakika kumi na tano zijazo benki ya TMB (Tikali Microfinance Bank) tawi la karibu jengo la Kamota Motorcycle, benki itavamiwa na kuporwa fedha zake zote, fedha za wana Tikali waliohifadhi mahali hapo zinakwenda kuchukuliwa na watu wasio na utu wala huruma ya kujua watu wa Tikali wamepambana vipi kuzipata fedha hizo. Taarifa hizi sijazitoa kwa chombo chochote cha Ulinzi na usalama kwani siwezi kushtaki kesi ya nyani kwa ngedere, vyombo vya Ulinzi na usalama mkiona kuna umuhimu wa ninyi kuokoa mamilioni ya wana Tikali kazi kwenu nendeni mkafanye kazi yenu ya kikatiba, ndugu zangu wasikilizaji kwa leo naomba tuishie hapo, tukutane wakati mwingine ahsanteni sana" Jonathan Sakewa alizima kipaza sauti chake na kufungulia muziki Kwa kuweka playlist kali ambayo wasikilizaji wanaopenda kukesha wazingepata shida ya burudisho la moyo, baada ya hapo alikagua milango yote na kuhakikisha kama imefungwa kisha aliufunga wa nje na kurejea kwenye gari lake, dereva aliondosha gari baada ya mita kadhaa walikutana na kizuizi cha magari mawili, dereva alitaka kugeuza gari na kutafuta njia nyingine. Jonathan Sakewa alimzuia asikimbie bali atulie, waliendelea kuyapa umakini magari ya mbele yao baada ya dakika mbili alirushuka mwanaume mrefu mwenye mwili mkubwa alishuka na kuwafuata, alitumia vidole kugonga kioo cha gari. Dereva alivuta bastola yake kuwa tayari kwa vulumai lolote ambalo watu hao wangeleta.
"Tulia kijana wangu, tulia tuwasikilize kwanza" Jonathan Sakewa alimzuia dereva kisha alimtaka afungue mlango wa upande wa kushoto aliokuwa yeye.
"Bila vurugu wala mapigano yoyote ya kuumizana naomba unifuate, mkuu anataka kuzungumza na wewe" mwanaume huyo alitoa amri.
"Mmmh MFF mmekuwa wa moto na haraka sana, huu muda mlionifuata hapa si mngeenda kuzuia fedha za wana Tikali siziende kwa mikono ya watu ambao hawatozipa thamani za matumizi kwangu hawajui zilipochumwa" Jonathan Sakewa aliongea huku akitabasamu wakati anashuka, alimgeukia dereva na kumtaka aondoke zake wala asimfuate. Jonathan Sakewa alimfuata mwanaume huyo mpaka kwenye gari mbili waliingia ndani yake na gari ziliondolewa kwa kasi eneo hilo. Huu ndio mwanzo wa kigongo chetu hiki naomba uwe pamoja nami mpaka mwisho.
HII SIMULIZI MPAKA MWISHO KWA TSH 3000 UNAWEZA KUISOMA, KARIBU WHATSAPP AU FACEBOOK NITEXT 0673049321
Advertisement
Event Venue & Nearby Stays
Kariakoo, Dar es Salaam, Tanzania